Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amewataka wakazi wa Mtwara kutoa ushirikiano Kwa bandari ya Mtwara ili iweze kutekeleza agizo la Rais la kusafirisha Korosho kupitia bandari hiyo.
Kanali Sawala ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu katika bandari hiyo ambapo amesema uwekezaji Mkubwa wa zaidi ya shilingi bilioni 157 uliofanywa na serikali umeiongezea bandari uwezo wa kusafirisha mizigo mingi zaidi tofauti na hali ilivyokuwa miaka michache iliyopita.
" Bila shaka Kila mmoja wenu anakumbuka hali ya usafirishaji ilivyokuwa kabla ya kuboresha miundombinu, hivi Sasa uwezo wa bandari yetu wa kusafirisha mizigo umepanda kutoka tani 400,000 hadi tani 1600, 000 Kwa mwaka" alisema Kanali Sawala.
Aidha Kanali Sawala ameongeza kuwa kutokana na ongezeko la uzalishaji wa zao la korosho katika msimu wa 2024/25 ni dhahiri kuwa hali ya uchumi wa wakazi wa Mtwara itaimarika huku akiwataka kuitumia vizuri fursa hiyo kujiletea Maendeleo.
Halikadhalika Kanali Sawala ameitumia fursa hiyo kutoa wito Kwa wafanyabiashara pamoja na wasafirishaji kuhakikisha korosho zote zilizoko katika maghala makuu zinasafirishwa hadi bandarini.
" Ndugu zangu tumeshuhudia jinsi uzalishaji wa korosho ulivyopanda, Sasa nitoe wito Kwa wadau wote wanaohusika na usafirishaji wa korosho kutoka kwenye maghala makuu kuharakisha mchakato wa kuzisafirisha mpaka bandarini" alisisitiza Kanali Sawala
Pia Kanali Sawala ameitumia fursa hiyo kumshukuri Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kuruhusu bandari ya Mtwara kusafirisha Korosho hatua ambayo amesema imechangia kutoa ajira sambamba na kuongeza pato la Mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.